Mhe. Jenista Joakim Mhagama (MB), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliwasili Cairo, Misri tarehe 31 Agosti, 2022 kuhudhuria Mkutano wa nne wa kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wanaoshughulikia masuala ya Utumishi wa Umma, Serikali za Mitaa, Maendeleo ya Miji na ugatuzi wa Madaraka (4th Ordinary Session of the Specialized Technical Committee on Public Services, Local Governments, Urban Development and Decentralization). Mkutano huu ulitanguliwa na mikutano ya wataalamu (Experts meetings) tarehe 29 na 30 Agosti, 2022.
Baada ya kufungwa mkutano huo, Mhe. Jenista Mhagama alifika Ubalozini Cairo na kupokelewa na Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na alipata fursa ya kuzungumza na Wafanyakazi wote wa Ubalozi.
Wakati wa mkutano huo alisisitiza haja ya kuimarisha mahusiano baina ya Misri na Tanzania ambayo yanazidi kukua siku hadi siku ili kumsaidia Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2025, pamoja na ndoto zake za kuimarisha Maendeleo ya Tanzania katika sekta zote.
Aidha, alieleza kuwa Misri ni nchi maalum ya kimkakati kwa Serikali ya Tanzania, hivyo, aliwasisitiza wafanyakazi wa Ubalozi kwa pamoja wamsaidie Balozi kwa kufanyakazi kwa uzalendo, bidii, ufanisi na uaminifu ili kufikia ndoto za Mhe. Rais Samia ya kupata maendeleo ya kasi kwa kuongeza wawekezaji zaidi, kuongeza nafasi za ajira, kuingiza fedha za kigeni kwa wingi na kufungua milango zaidi ya biashara kati ya nchi hizi mbili.
Mwisho, Mhe. Jenista Mhagama aliwahakikishia watumishi wa Ubalozi kuwa Serikali inajitahidi kuimarisha mifumo mbali mbali ili kusimamia utumishi wa umma, lengo ni kupata watumishi wenye kuleta tija na ufanisi kuweza kupima mchango wa kila mtumishi Serikalini kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake.
Hivyo, alitoa wito kwa Mhe. Balozi na wafanyakazi wote wa Ubalozi kuzingatia imani ya Mhe. Rais kwao na kumsaidia kadri iwezekanavyo kutimiza ndoto zake kuibadilisha Tanzania kimaendeleo kupitia mifumo mbali mbali (Digital Government), kwa kuitangaza nchi yetu na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia