Tarehe 23 Januari, 2025 Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri akiwa na Maafisa wa Ubalozi, Maafisa kutoka TIC, Wizara ya Kilimo, TPA na Sekta binafsi kupitia TCCIA, amefanya kongamano kubwa la kuhamasisha uwekezaji nchini Tanzania, lilofanyika Sofitel Hotel. Cairo.

Kongamano hilo lililopewa jina la " Tanzania-Egypt Business Forum, lengo lake ni kutangaza fursa mbali mbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania katika Sekta ya Viwanda, ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, utalii, kilimo biashara, afya, teknolojia ya habari na nishati ili kuvutia Wawekezaji kutoka Misri kuwekeza mitaji yao nchini Tanzania.

Kongamano hilo limehusisha Makampuni Makubwa nchini Misri kama vile Elsewedy Electric na Arab Contractors ambayo tayari yamewekeza Tanzania.

Aidha, Mamlaka ya Uwekezaji nchini Misri nayo imesema iko tayari kuyakaribisha Makampuni yaliyopo Tanzania kibiashara na uwekezaji nchini Misri ili kunufaika na soko kubwa lililopo pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuboreshwa kila uchao.

Mhe. Balozi alisisitiza umuhimu wa kongamano hilo kama ni hatua muhimu ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na biashara baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Misri kutokana na azma ya pamoja ya kuimarisha mahusiano ya nchi na nchi, pamoja na kufungua fursa kwa manufaa ya pande zote, Tanzania na Misri.