Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, akiwa na ujumbe wa Tanzania uliofika Misri kuhamasisha uwekezaji nchini Tanzania unaoongozwa na Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania, tarehe 26/1/2025 ametembelea Kiwanda cha SILO Foods for Food Industries kinachomilikiwa na Wizara ya Uzalishaji Jeshini nchini Misri kilichopo Sadat City, Alexandria.

Kiwanda hicho kinazalisha bidhaa mbali mbali zinazotokana na zao la ngano kama vile mikate ya aina tofauti, Biskuti, Makaroni  na ngano nzima iliyokobolewa.

Pia, kiwanda hicho huzalisha maziwa pamoja na vifungashio vya bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo zinazouzwa ndani na nje ya Misri.

Pamoja na kusafirisha nje bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda hicho, pia ndio wenye jukumu la kutoa chakula kwa Wanafunzi nchini Misri kwa kuzingatia lishe inayohitajika kulingana na umri wa mtoto kama wanavyopewa miongozo na Wizara ya Afya hapa nchini.

Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe aliwakaribisha wawekezaji hao nchini Tanzania kuwekeza ili kuongeza thamani mazao ya kilimo ikiwa pamoja na Korosho na Karafuu zinazozalishwa kwa wingi Tanzania. Alisema, pia zipo fursa nyingi katika sekta ya ujenzi, utalii na viwanda vya aina mbali mbali.

Uongozi wa kiwanda hicho umeahidi kuendeleza mazungumzo ili kuwekeza Tanzania. Ujumbe wa Tanzania upo Alexandria Misri kufanya kongamano kubwa uwekezaji tarehe 27/1/2025 litakalofanyika ukumbi wa Alexandria Chamber of Commerce.