Tarehe 07 Julai, 2025 Ubalozi wa Tanzania nchini Misri umeadhimisha siku Lugha ya ya Kiswahili Duniani kwa mafanikio makubwa ambapo vijana wa Misri walionesha umahiri wao mkubwa katika kukitumia Kiswahili katika Sanaa ya ushairi, utenzi, mazungumzo na muziki wa kizazi kipya, muziki wa dansa n.k.
Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri amesisitiza haja kwa Mabalozi wa Nchi za Afrika kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kuleta Amani, umoja, na mshikamano na kuondosha tofauti zilizopo.
Naye Mhe. Omar Ntezimbere, Balozi wa Burundi nchini Misri alieleza kuwa Kiswahili ni lugha inayokuwa haraka Kimataifa inayozungumzwa na watu zaidi ya milioni 250. Hii ni kwa sababu Kiswahili hakijui mipaka ya nchi, haijui kabila Bali inahitaji upendo tu ili uweze kuizungumza.
Maadhimisho hayo yalifanyika Hoteli ya Pyramisa mjini Cairo na yalihudhudhuriwa na Dkt. Aliaa Burhan, Kaimu Msaidizi wa,Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Utamaduni ambaye ndiye alikuwa mgeni Rasmi. Wengine ni pamoja na Balozi Mohamed Swafat anayeshughulikia nchi za Bonde la Mto Nile, Balozi wa Cameroon, Rwanda na wawakilishi wa Mabalozi kutoka nchi za Afrika Mashariki. Maadhimisho hayo yamefanywa kwa ushirikiano mkubwa na ubalozi wa Burundi chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Umoja wa Mabalozi wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) waliopo Cairo nchini Misri.