Mhe. Balozi Ziarani Mkoani Alexandria

Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo. Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri alifanya ziara ya kikazi mjini Alexandria tarehe 6 na 7 Machi, 2025 kwa kutembelea Maktaba Kuu ya Alexandria, baadae alitembela hospitali inayomilikiwa na Taasisi ya Nile of Hope, Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa huduma za afya bure kwa watoto wanaozaliwa na ulemavu wa viungo ikiwa ni pamoja na matatizo ya moyo.

Uongozi wa hospitali hiyo pia umekuwa ukiandaa Kambi tiba tokea mwaka 2014  hadi mwaka 2019 nchini Tanzania katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam na Mnazimmoja - Zanzibar kwa kutoa tiba za upasuaji wa matatizo ya kiafya kwa watoto. Taasisi hiyo inakusudia kujenga hospitali ya Kisasa Zanzibar endapo itapatiwa ardhi, pamoja na kuendeleza mpango wa Kambi Tiba katika mikoa na Wilaya nchini Tanzania.

Aidha, tarehe 7 Machi, 2025 Mheshimiwa Balozi Alikutana na Madaktari bingwa kutoka Tanzania wanaosoma katika fani mbali mbali za ubobezi na Matibabu Chuo Kikuu cha Alexandria. Pia. Mkutano huo uliwajumuisha Wahandisi wanaosoma Chuo cha Egypt - Japan University of  Science and Technology (E-JUST) na Maafisa Wahandisi wa Jeshi la Wananchi wanaosoma vyuo mbali mbali vya Jeshi nchini Misri.

Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano baina ya Maktaba ya Alexandria na Taasisi za  Kielimu na Makumbusho za Tanzania. ikiwemo pia kuimarisha ushirikiano na Taasisi ya Nile of Hope ili kuendeleza Sekta ya Afya nchini Tanzania. 

Vilevile ziara ililenga kufahamu maendeleo ya Watanzania walioko Alexandria, kujua changamoto zao ili ubalozi uweze kuzifuatilia na kupatiwa ufumbuzi wake. Mheshimiwa Balozi amerejea Cairo tarehe 8 Machi, 2025 asubuhi baada ya kukamilisha ziara hiyo.