Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri umeadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioasisiwa rasmi tarehe 26 Aprili, 1964. Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika tarehe 26 Aprili, 2025 katika Hoteli ya Pyramisa, Mjini Cairo, Mhe. Balozi Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo alieleza furaha yake kujumuika pamoja na Mabalozi na wawakilishi wa Mabalozi wa nchi za Afrika ya Mashariki, wawakilishi wa Serikali ya Misri, wawakilishi wa Makampuni na wawekezaji kutoka Misri, kuadhimisha miaka 61 ya mafanikio ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii yaliyopatikana nchini Tanzania.
Aidha, Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi unaokuwa kwa asilimia 6 hadi 7 ndani ya miaka 10 iliyopita na kuifanya Tanzania kuwa na uchumi unaokuwa kwa kasi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki.
Vilevile, alieleza kuwa mbali ya kutimiza miaka 61 ya Muungano, pia Tanzania inasherehekea kuwa kielelezo cha umoja, amani na utulivu sio tu Barani Afrika, bali pia Duniani kote.
Naye, Balozi Mohamed Safwat Atta, Mwakilishi kutoka Serikali ya Misri alisema kuwa Muungano wa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika kudumisha umoja, utulivu na mshikamano Barani Afrika na Duniani kote.
Pia uhusiano wa Tanzania na Misri umepewa kipaumbele nchini Misri katika kuuimarisha na Viongozi wa juu wamekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja. Aidha, mradi wa ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere ni kielelezo cha ushirikiano wa kimaendeleo yanayohitajika Barani Afrika.
Nchi za Afrika zimeaswa kuunganisha nguvu zao, utaalamu, rasilimali na mshikamano wao kujiletea maendeleo kwa kufanyakazi pamoja na kubuni miradi mikubwa ya maendeleo, kwa misingi ya kuheshimiana, kuheshimu sheria za ndani za nchi zao na sheria za Kimataifa ili kuleta maendeleo ya nchi na Bara la Afrika kwa ujumla.
Pia, alisisitiza haja ya kutumia vyema uwepo wa Tanzania na Misri katika eneo la kimkakati Kijiografia katika kukuza biashara, uwekezaji na uendelezaji wa miradi ya kimkakati ya Bandari, miundombinu, nishati, kilimo na mawasiliano kwa ujumla.