Mheshimiwa Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, emeonana na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 12 wa World Urban Forum (WUF12) wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Lucy D. Kabyemera Washiriki hao kutoka Wizara ya Ardhi, Dar Rapid Transit Agency (DART), Shirika la Nyumba Tanzania na TAMISEMI, walielezea kufurahishwa kwao na maendeleo ya Misri katika sekta ya miundombinu na Ujenzi, ambapo walionyesha nia ya kurejea nchini Misri kujifunza mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya Miji, makazi na mifumo ya usafirishaji pamoja na utekelezaji wa miradi mbali mbali ya makazi, uendelezaji wa Miji mipya na mipango miji kwa ujumla.
Na mnamo tarehe 07 Novemba, 2024, Mheshimiwa Balozi alifika katika Banda la Tanzania katika Ukumbi wa Mikutano ambapo alipewa maelezo ya Manufaa ya ushiriki wa Tanzania pamoja na kuutangaza mradi wa DART unaotoa huduma za usafiri wa Umma nchini Tanzania ulioweza kupunguza foleni kwa asilimia 50 nchini Tanzania.
Mkutano wa WUF12 utafungwa rasmi tarehe 08 Novemba, 2024 ambapo jumla ya washiriki 30 kutoka Tanzania walishiriki. Ubalozi umewapongeza washiriki hao kwa kuiwakilisha vyema Tanzania na amewakaribisha tena kurejea Misri kwa kupata taaluma mbali mbali kuhusu mipango miji, usimamizi na maendeleo ya makazi kwa ujumla.
Aidha, Bi. Lucy D. Kabyemera alitoa shukrani zake kwa Ubalozi kwa mapokezi mazuri na ushirikiano walioupata katika kufanikisha ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo.
Mwisho, aliwatakia safari njema kurejea Nyumbani Tanzania na ubalozi unasubiri kupokea maombi mbali mbali kutoka Taasisi wanazoziwakilisha, kwa ajili ya kupata mafunzo mbali mbali ya kujengewa uwezo kutoka Serikali ya Misri.