Tarehe 20 Agosti, 2024 Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri amewapokea wakaguzi wanne kutoka Taasisi ya Medical Store Department (MSD) wakiongozwa na Bibi Batuli M. Mushi, Afisa wa Sheria Mwandamizi wa MSD waliofika Cairo kwa kazi ya ukaguzi wa Kampuni ya Hefny Phatmaceutical Group inayotarajia kuwekeza kiwanda cha utengenezaji wa  Medical Gloves na Medical Cotton nchini Tanzania. 

Ukaguzi wa Kampuni hiyo umeanza tarehe 20 hadi 26 Agosti, 2024 ikiwa ni juhudi za utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi na Viwanda katika sekta ya Afya.

Misri ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya Afya ambapo zaidi ya viwanda 200 vya dawa vinazalisha dawa za aina mbali mbali zenye ubora wa hali ya juu na zenye unafuu mkubwa wa bei.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Balozi amewapokea viongozi wa Scout kutoka Tanzania wakiongozwa na Bw. Rashid K. Mchatta, Scout Mkuu waliofika Ubalozini kumsalimia Balozi.

Viongozi hao wapo Misri kuhudhuria Mkutano wa 43 wa 'World Scout Conference' uliofunguliwa rasmi tarehe 17 Agosti, 2024 katika ukumbi wa Al Qobba Palace, saa 2 usiku na Mhe. Moustafa Madbouli, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri chini ya usimamizi wa Mhe. Abdel Fattah El- Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri.