Tarehe 22-07-2024 Mhe. Maj. Gen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri alifanya mazungumzo na Mhe. Sergio Nathu CABA, Balozi wa Jamhuri ya Msumbiji nchini Misri kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji.

Balozi Makanzo alieleza kuwa nchi ya Msumbiji ni zaidi ya jirani kutokana na urafiki wa muda mrefu uliopo tokea enzi za harakati za ukombozi wa nchi za Afrika.

Aidha, urafiki na undugu uliopo unazidi kuimarika ambapo Rais wa Msumbiji alifanya ziara nchini Tanzania iliyopelekea kutiwa saini makubaliano mbali mbali ikiwa ni pamoja na biashara katika mipaka ya nchi hizi mbili.

Hivyo, alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa kufanyakazi pamoja kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha ustawi wa wananchi kutokana na hofu inayojengwa na wanaotekeleza vitendo vya kigaidi.

Balozi Makanzo aliwatakia mafanikio wananchi wa Msumbiji katika chaguzi za Rais,  Wabunge na Magavana zinazotarajiwa kufanyika Oktoba, 2024.

Aidha, Balozi Sergio CABA alipongeza mahusiano na mashirikiano mazuri yaliopo baina ya Tanzania na Msumbiji pamoja na juhudi za kusaidia mapambano dhidi ya ugaidi katika Jimbo la Cabo Delgado.

Pia Balozi Sergio aliitakia Tanzania mafanikio katika chaguzi za Rais, Ubunge na Serikali za Mitaa zitakazo fanyika mwakani 2025.

Kwa pamoja viongozi hao walisisitiza haja ya kubadilishana taarifa na uzoefu, kufanyakazi kwa pamoja na kushauri haja ya vyama vya ukombozi katika nchi za Kusini mwa Afrika kukaa pamoja kujadili namna ya kushirikiana zaidi ili kuimarisha nguvu ya pamoja katika kuendeleza mapambano dhidi ya maadui wa Bara la Afrika katika kulinda uhuru, umoja na amani barani Afrika.