Mkuu wa Utawala (HOC) ambaye pia ni Kaimu Balozi Ndg.  Makame Iddi Makame,  -akiambatana na maafisa wa Ubalozi Bw. Thabit A. Othuman, Mwambata Fedha  na Bi. Nimpha E. Marunda, Mwambata Utawala - alikutana na uongozi wa Kampuni ya GIT-ZONE International katika mji wa Nasr City tarehe 03 Agosti  2023, kwa kengo la kuimarisha mahusiano na kampuni hiyo. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Osama Fahmy alieleza kuwa kampuni yao inajishughulisha na biashara za kimataifa ambapo imekuwa na mashirikiano na Makampuni makubwa duniani pamoja na wawekezaji wakubwa duniani kutoka nchi za Ulaya, Ghuba na Afrika. Lengo la kampuni ni kuwaunganisha wawekezaji, kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa, kusaidia utekekezaji wa miradi pamoja na usafirishaji wa bidhaa mbali mbali (Import and Export). 
Aidha, ilieleza kuwa Kampuni hiyo kwa sasa inaiangalia Tanzania kama ni Kimbilio na kitovu cha Uwekezaji katika Afrika ya Mashariki na iko tayari kusaidia uwekezaji katika sekta mbaki mbali kwa kuanzia sekta ya elimu, usafirishaji na ujenzi. 
Pia, kampuni hiyo husaidia makampuni mengine kupata fedha za utekekezaji wa miradi yao, kutafuta washirika katika kutekeleza miradi, kufanya Mikutano ya kimataifa kwa kuwakutanisha wawekezaji kutoka sehemu mbali mbali Duniani, pamoja na watendaji wa Serikali na Sekta binafsi kujadili changamoto na mafanikio katika masuala ya biashara na uwekezaji kwa ujumla.
Ubalozi tayari umeshaiunganisha Kampuni hiyo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambapo kikao cha mwanzo kimefanyika kwa njia ya mtandao kupata ufafanuzi wa masuala mbali mbali kuhusu uanzishaji wa Kampuni Tanzania, mfumo wa kodi, na manufaa mbali mbali ya uwekezaji nchini Tanzania.
Kampuni hiyo inakusudia kufanya kongamano la pili la siku ya uwekezaji Kimataifa Barani Afrika (Africa Investment Day) ifikapo Machi, 2024 Tanzania ikiwa Serikali itaridhia ombi la Kampuni hiyo baada ya kuwasilisha andiko dhana (concept note) kuhusu nia ya Kampuni Hiyo. 
Ubalozi uliwakaribisha Viongozi wa Kampuni hiyo kufanya ziara nchini Tanzania na kuonana na Viongozi mbali mbali wanaohusika na Uwekezaji na biashara kwa ujumla. Aidha, walielezwa kuwa zipo taasisi za wafanyabiashara katika sekta binafsi ambao wanaweza kukutanishwa kubadilishana uzoefu, taarifa na kufanya ubia kwa utekekezaji wa miradi mbali mbali. 
Mwisho  uongozi wa Kampuni hiyo umekubali kufanya ziara Tanzania baada ya kuwasilisha andiko dhana na kuahidi kuto tarehe inayopendekezwa kufanyika ziara hiyo ndani ya muda mfupi ujao.