Tarehe 06 Novemba, 2024, saa 2:00 usiku Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, alifika uwanja wa 30th June, Stadium uliopo New Cairo, nchini Misri kushuhudia pambano la kirafiki baina ya Timu ya Taifa ya Vijana wa Kiume chini ya miaka 20 dhidi ya Timu ya Taifa ya Misri ya Vijana chini ya miaka 20.
Mchezo huo ulikuwa mzuri ambapo hakuna aliyetoka kifua mbele katika mchezo huo, baada ya kutoka bila ya kufungana. Mara baada ya kumalizika mchezo huo, Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, alipata fursa ya kuzungumza na wachezaji pamoja na Viongozi wa Timu na Makocha wao ambapo aliwapongeza kwa mchezo mzuri waliouonyesha yaliyopelekea kutoka sare bila ya kufungana.
Alieleza kuwa, vijana wamejituma na upo uwezo wa kushinda mechi yao ya pili huko Ismailiya, nje kidogo ya Cairo siku ya tarehe 09 Novemba, 2024.
Aidha, aliwapongeza Viongozi na Makocha kwa maelekezo yao mazuri na kuwatakia mafanikio mazuri katika ziara yao hiyo na kwamba ipo haja kuzialika Timu za Misri nchini Tanzania ili kuimarisha Urafiki na diplomasia kupitia sekta ya michezo.