Tarehe 15/02/2024 Mhe. Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri alimtembelea Mhe. Diab Allouh, Balozi wa Palestina nchini Misri kwa lengo la kujitambulisha rasmi pamoja na kuimarisha uhusiano.

Aidha, ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Taifa la Palestina ikiwa ni pamoja na kuimarisha biashara na uwekezaji katika kuimarisha Viwanda, Kilimo, utalii, sekta ya uchukuzi pamoja na madini.

Mhe. Balozi alifahamisha kwamba uhusiano baina ya Tanzania na Taifa la Palestina ni wa kihistoria wakati wa harakati za ukombozi ambapo Tanzania ililitambua Taifa la Palestina mapema sana.

Mhe. Balozi Richard Makanzo alimfahamisha Balozi Diab uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania pamoja na rasilimali nyingi za madini, maliasili za maji ya kutosha kusaidia uwekezaji katika kilimo, uwepo wa vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, wanyama pori wanaohama kutoka Tanzania kwenda Kenya na kurejea Tanzania pamoja na fukwe nzuri za Bahari ya Hindi katika Visiwa Vya Zanzibar, inayozungukwa na Hoteli kubwa za kisasa.

Naye Balozi Diab Allouh alitoa shukurani zake kwa kutembelewa na Balozi Richard na kusema kuwa Ubalozi wa Palestina daima unathamini haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Tanzania na kwamba uko tayari kushirikiana naye akiwa ni Balozi wa Tanzania nchini Palestina mwenye makazi yake Cairo nchini Misri.

Aidha, Ubalozi uko tayari kushirikiana na Tanzania katika kila sekta na kwamba uratibu utafanywa kufanya ziara na kundi la Wafanyabiashara kutoka Palestina kwenda Tanzania.

Kisiasa, Balozi Diab aliiomba Tanzania kuendelea kuiunga mkono Palestina katika majukwaa ya Kimataifa ili kufikia lengo la utatuzi wa mgogoro unaoendelea na hatimae kufikia suluhisho la kuundwa kwa mataifa mawili, Taifa la Palestina na Taifa la Israel kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1948 ambapo Jerusalem ya Mashariki itakuwa ndio mji Mkuu wa Palestina.