Tarehe 06 Februari, 2024 Mhe. Mej. Gen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri akiwa na Timu ya wakaguzi wa Dawa na Vifaa Tiba kutoka Tanzania Medicines and Medical Devices Authority (TMDA) waliopo Misri kwa kazi ya ukaguzi wa viwanda vya dawa, alihudhuria kikao maalum cha ushirikiano na Egyptian Drugs Authority (EDA) ili kwa pamoja kujenga uhusiano na ushirikiano katika udhibiti wa dawa na vifaa tiba ili kufanyakazi kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na mafunzo kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa.

Mkutano huo uliowakutanisha Maafisa watendaji Wakuu wa Viwanda vya dawa nchini Misri, kiliongozwa na Dr. Ali Ghamrawy, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa nchini Misri (EDA) akiwa na Maafisa Waandamizi wa Mamlaka hiyo, Mhe. Mej. Gen. Richard M. Makanzo naye akiwa na Bw. Adam M. Fimbo, Mkurugenzi wa TMDA anayeongoza timu ya Wakaguzi kutoka Tanzania wanaokagua viwanda vya dawa nchini Misri.

Uongozi wa TMDA umewasilisha nakala ya awali (draft) ya Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya TMDA na EDA hatua ambayo itasaidia kuharakisha kazi ya usajili wa dawa zinazozalishwa Tanzania kuingia Misri na zile zinazozalishwa Misri kuingia Tanzania, soko la Afrika Mashariki na SADC kwa ujumla.

Aidha, ushirikiano huo utafungua milango ya uwekezaji wa viwanda vya Dawa kwa wingi nchini Tanzania kutoka kwa wawekezaji kutoka nchini Misri.

Jumla ya viwanda vya dawa 200 vimesajiliwa nchini Misri vinavyotosheleza soko la ndani la asilimia 94 na sasa vinahitaji kuongeza uzalishaji kukidhi soko la Tanzania, Soko la Afrika Mashariki na SADC kwa ujumla.