Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El Sisi leo tarehe 24/04/2024 ametuma ujumbe maalum kwa kumtuma Afisa kutoka Ikulu Bw. Mohamed Mokhtar kuwasilisha salamu za pongezi za kutimiza miaka 60 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwenda kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bw. Mohamed Mokhtar alipokelewa na Bw. Rashid S. Haroun (Kaimu Balozi) na Bi. Nimpha E. Marunda (Mwambata Utawala) katika Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri.

Nae Mhe. Rashid S. Haroun alizipokea salamu hizo kwa niaba ya Mhe. Balozi wa Tanzania nchini Misri Mej. Gen. Richard M. Makanzo na kutoa shukurani kwa niaba yake.

Aidha, katika yaliyojiri wakati wa  kupokea ujumbe huo ni pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mahusiano mema na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Misri na kuzidi kuuimarisha katika nyanja zilizopo za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kiuwekezaji, utalii, afya,ulinzi na usalama,elimu na michezo.

Ikumbukwe kuwa tukio la Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar lina historia kubwa na muhimu kati ya Tanzania na Misri kwani katika mwaka huo wa 1964 Tanzania pia ilifungua kwa mara ya kwanza ofisi za Ubalozi nchini Misri na Balozi wa kwanza akiwa Mhe. Salim Ahmed Salim, hivyo katika maadhimisho haya Tanzania na Misri zinasherehekea miaka 60 ya ushirikiano.