Mhe. Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri tarehe 22/03/2024 alikutana na Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Vyuo mbali mbali vilivyopo Alexandria kujua maendeleo yao, kupata mrejesho wa mambo mbali mbali waliyomuomba kuwasaidia alipokutana nao Mwezi Januari, 2024.

Pia aliweza kujumuika nao pamoja katika chakula cha pamoja katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika hoteli ya Stegeinberger, iliopo Alexandria.

Nae Bw. Alihussein, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi wanaosoma Alexandria alitoa shukurani kwa Balozi na timu yake kwa ufuatiliaji mzuri wa matatizo yao baada ya kuyafikisha sehemu husika ikiwa ni pamoja na kupunguziwa ada ya masomo kutoka Dola za Marekani 1,500 hadi Dola 300.

Aidha, wamepata mrejesho wa Udhamini kupitia Dr.Samia Superspecialized Scholarship ambapo Wanafunzi waliokosa mwanzo wametakiwa kuomba tena baada ya fursa hizo kutangazwa.

Akitoa nasaha zake kwa Wanafunzi hao, Mhe. Balozi alisisitiza umoja, upendo, bidii na kusaidiana katika masomo yao ili kila mmoja wao afaulu na kuendeleza umoja wao hata wanaporejea Tanzania wakiwa katika majukumu yao Sehemu mbali mbali.

Wanafunzi walioko Alexandria wanasoma kozi za udaktari bingwa katika maradhi mbali mbali na upasuaji, unesi, Maafisa wa Jeshi wanaosoma kozi za Nevi, Maafisa Kadet, ulinzi wa anga, chemical explosive engineering na wanafunzi wa uhandisi wa Environmental Engineering katika chuo cha Egypt-Japan University of Science and Technology (E-JUST).Baadhi ya wanafunzi hao wanatarajia kumaliza masomo yao mwezi Oktoba, 2024.

Wakati huo huo, Mhe. Balozi aliwasihi Madaktari hao bingwa kufanya tafiti na kuwasilisha mapendekezo yao ubalozini juu ya mikakati inayoweza kutumika kupambana na maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya Ini, Figo, Kisukari, magonjwa ya Moyo ili kuisaidia Serikali kupambana na kutokomeza kabisa magonjwa hayo nchini Tanzania, magonjwa ambayo yanaonekana kuwa tishio miongoni mwa Vijana wengi nchini Tanzania.

Aliwasihi kutumia vyema taaluma zao kulinda taifa kwa kuwekeza katika afya za Watanzania, rasilimali muhimu katika kujenga uchumi wa nchi, uwekezaji, biashara na kuendeleza uhusiano kwa ujumla. Hii ni kwa sababu Misri imefanikiwa sana kupambana na maradhi ya Ini na wanao ujuzi mkubwa katika sekta ya afya, hivyo ipo haja kuwasaidia Watanzania kwa kuongeza idadi ya wataalamu wanaopata mafunzo nchini Misri pamoja na kuweka mikakati imara kupambana na maradhi mbali mbali nchini Tanzania.