Mheshimiwa Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri tarehe 02/09/2024 amekutana na Uongozi wa Jumuiya ya Wahandisi nchini Misri chini ya uongozi wa Mhandisi Meja Jenerali Mohamed Naaser Hussein Badr, Mjumbe wa Bodi ya Wahandisi Waandamizi waliofika Ubalozini kuzungumzia haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Wahandisi wa Tanzania kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania.

Uongozi huo wa Jumuiya ya Wahandisi nchini Misri ulieleza kuwa ipo haja ya kufufua upya ushirikiano na uhusiano baina ya Jumuiya hizo mbili kupitia makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini mwaka 2017 kwa kubadilishana ziara za kutembeleana kwa mafunzo, kubadilishana uzoefu, kubadilishana tamaduni, kufanya mikutano na makongamano ya pamoja, kushirikiana katika utekelezaji wa kazi na miradi mbali mbali pamoja na kuandaa ziara za Makampuni mbali mbali kutembeleana na kujifunza.

Aidha, nae Mheshimiwa Balozi aliupongeza uongozi wa Jumuiya hiyo kwa maono yao ya kuimarisha Taaluma ya uhandisi kwa kuboresha makubaliano ya ushirikiano na kusisitiza haja ya kutoa mafunzo kwa vijana wanaomaliza Vyuo Vikuu katika fani hiyo ya uhandisi pamoja na kuwapatia mafunzo wahandisi pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji katika ngazi za fundi mchundo waliomo makazini katika taasisi mbali mbali ili kupata wataalamu wengi wenye ujuzi wa kutengeneza zana mbali mbali za kazi, vipuri na mitambo.

Pia, alisisitiza haja ya kuanzisha miradi mikubwa ya viwanda na taasisi za ufundi kwa ushirikiano na Serikali au Taasisi binafsi ili kuongeza thamani bidhaa mbali mbali za kilimo, mifugo na kadhalika kwa kushirikiana na Taasisi ya Arab Organization for Industrialization (AOI) yenye viwanda zaidi ya 15 vinavyozalisha bidhaa mbali mbali kwa matumizi ya jeshini, jamii na huduma kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Mohamed Naaser alifuatana na Mhandisi Mkongwe Bw. Ahmed Hesham, Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wahandisi nchini Misri ambaye alimkabidhi Balozi vitabu viwili kuhusu historia ya Uhandisi nchini Misri na Uingereza.

Tutarajie mafanikio makubwa kwa Watanzania kupitia ushirikiano huu kwa maendeleo ya Taifa letu.