Tarehe 01 Agosti, 2024 Mhe. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri amekutana na Mhe. Khaled Atef Abdul Ghaffar, Naibu Waziri Mkuu na pia Waziri wa Afya na Maendeleo ya Watu nchini Misri huko Alamein City, nje kidogo ya Cairo kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano Baina ya Tanzania na Misri kupitia sekta ya Afya.

Mhe. Balozi Makanzo aliiomba Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kutumia nafasi yake kumuunga mkono mgombea  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika katika Shirika la Afya Ulimwenguni katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Congo, Brazzaville, mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti, 2024.

Aidha, Mhe. Balozi Makanzo alizungumzia suala la ushirikiano katika kupambana na maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na maradhi ya Ini, (Hepatitis B, C, ) Figo, kisukari, kansa na kadhalika.  

Kwa upande wake, Mhe. Khaled Atef Abdul Ghaffar, alimuhakikishia Balozi Richard Makanzo kwamba Misri itajitahidi kutumia ushawishi wake kupitia majukwaa mbali mbali kuhakikisha mgombea wa Tanzania katika Shirika la Afya Duniani anapata kura nyingi kushinda nafasi hiyo. 

Kama ambavyo Mhe. Naibu Waziri Mkuu ameahidi kutoa nafasi za mafunzo kwa Madaktari wa Tanzania kuja Misri kujifunza namna ya kupambana na maradhi ya ini hatua kwa hatua na namna ya kuwatambua Wagonjwa na udhibiti wa Ugonjwa huo kabla haujakomaa.

Pia, Mhe. Khaled amemwalika Waziri wa Afya wa Tanzania kufanya ziara nchini Misri kuhudhuria mkutano utakaofanyika Oktoba, 2024.

Wakati huo huo, walijadiliana katika kushirikiana namna ya kupambana na Magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na imeshauriwa kwa Tanzania kusomesha wataalamu wake wa Afya ili kuweza kudhibiti maradhi mbali mbali yasiyoambukiza kwa kutumia utaalamu na uzoefu wa madaktari bingwa wa Misri, pamoja na kufanya kambi tiba nchini Tanzania ambapo Madaktari bingwa watapelekwa nchini Tanzania baada ya kupokea mahitaji mbali mbali ya mafunzo na wataalamu wanaohitajika kutoa huduma za tiba nchini Tanzania.