Tarehe 31 Oktoba, 2024 Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri katika jitihada za utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi ameitembelea kampuni ya Precision Consulting Engineering ya Misri inayojishughulisha na Kazi za uchoraji, ujenzi na usimamizi wa ujenzi wa majengo ya kisasa kwa makazi na biashara. 

Kampuni hii yenye uzoefu wa miaka 16 sasa, imefungua Ofisi zake za Kanda nchini Misri, Saudi Arabia, Italy, Umoja wa Falme za Kiarabu na sasa inakusudia kufungua Ofisi yake nchini Tanzania kuhudumia soko la Afrika kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika. 
Kampuni hii inaongozwa na Mwenyekiti akisaidiwa na Wakurugenzi mbali mbali wa vitengo. Mheshimiwa Balozi ameipongeza Kampuni hii kwa mafanikio makubwa kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa na mingi katika nchi mbali mbali za Ulaya na Mashariki ya Kati, hali inayoonyesha kuaminiwa kwa kampuni, uwepo wafanyakazi hodari wenye ujuzi na utendaji kazi wenye ufanisi mkubwa.

Kampuni hii ilifahamishwa uwepo wa fursa mbali mbali nchini Tanzania katika sekta ya uchumi wa buluu, ujenzi wa miundombinu, nyumba za makazi na biashara pamoja na uwekezaji sekta ya utalii.
Aidha, Mheshimiwa Balozi aliwasihi wawekezaji hao kutumia fursa hiyo kuitembelea Tanzania kujionea vivutio mbali mbali vya utalii ikiwa ni pamoja na Mlima mrefu zaidi Barani Afrika, mlima Kilimanjaro, kujionea mbuga za Wanyama, visiwa vya Zanzibar vyenye fukwe nyeupe na visiwa vidogo vidogo vingi kwa ajili ya uwekezaji. 

Bw. Walked Sweida, Mwenyekiti, alifahamisha kuwa Kampuni yake imepanga kutembelea Tanzania Tarehe 3 Novemba, 2024 kuona fursa mbali mbali za uwekezaji ambapo ziara itakamilika kwa kufika Zanzibar na kwamba ubalozi uneombwa kusaidia ufanikishaji wa ziara hiyo nchini Tanzania.

Wakati huo huo, tarehe 30 Oktoba, 2024, Mhe. Balozi alifanya ziara katika mji wa Sokhna, nje kidogo ya Cairo kuikagua Kampuni ya Sokhna Auto Park Company inayojishughulisha na uingizaji na usafirishaji wa magari ya aina mbali mbali yaliyotumika, ndani na nje ya Misri. Kampuni inakusudia kuingia katika soko la Tanzania kwa biashara ya magari ya aina mbali mbali.