Tarehe 24-07-2024 Mabalozi wa nchi za SADC waliopo Cairo wametembelea miradi ya kilimo cha matunda, mbogamboga na uzalishaji wa maziwa katika mji wa Sadat City, huko Alexandria.
Lengo la ziara hiyo ni kujifunza kwa vitendo kilimo cha kisasa cha umwagiliaji maji, uvunaji wa maji ya chini ya ardhi na kuyatumia kwa kilimo na ufugaji wa Samaki.
Pamoja na teknolojia ya kisasa katika mazingira ya jangwa. Ziara hiyo ilianza kwa kutembelea kampuni ya Gelila for Import and Export na Ragab Group zinazozalisha matunda mbali mbali ikiwa ni pamoja na Zabibu, machungwa, chenza, malimau, makomanga na kadhalika na kusafirisha nchi mbali mbali duniani.
Aidha, ziara ilikamilika kwa kutembelea shamba la mifugo ya Ng'ombe na nyati kwa ajili ya maziwa, nyama na bidhaa mbali mbali za maziwa kama mtindi na siagi.
Mabalozi hao waliridhishwa na taaluma waliyoipata ambapo mipango ya kuingia katika ushirikiano na sekta binafsi katika nchi zao na makampuni hayo zitafanywa ili kuutumia utaalamu wa kilimo wa Misri na kueneza katika nchi mbali mbali barani Afrika.
Pia, ziara hiyo imeongeza na kuimarisha zaidi mahusiano na mashirikiano na nchi za SADC ambapo Wizara ya Kilimo Idara ya utafiti imeahidi kuwa karibu zaidi na Mabalozi hao katika utekelezaji wa kazi zao nchini Misri.