Mhe. Maj Gen Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mashirikiano na Diaspora, waliopo Misri, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Al Azhar, Cairo, Ain Shams na Aswan pamoja na wanafunzi wa Misri wanaosoma Kiswahili katika Vyuo hivyo, ameadhimisha siku ya Kiswahili Duniani kwa mafanikio makubwa.
Maadhimisho hayo yalipambwa kwa tenzi, mashairi na nyimbo zilizoimbwa na wanafunzi wanaosoma Kiswahili.
Aidha, Mabalozi wa nchi za Afrika Mashariki waliohudhuria kutoka Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya na D.R. Congo ambao walisisitiza haja ya kukiendeleza, kukifundisha, kukisambaza na kukienzi Kiswahili Lugha pekee ya Bara la Afrika iliyokubalika rasmi kutumika Kimataifa ili kuimarisha umoja wetu, kufundisha utamaduni wetu na mila zetu ili kuleta umoja, amani na maendeleo kwa ujumla Barani Afrika.
Mhe. Balozi alitoa zawadi za Kamusi na vitabu vya kufundishia Kiswahili kwa vyuo vikuu vya Misri, ngao kwa vyuo hivyo na Redio Cairo kutambua mchango wao mkubwa wa kufundisha na kukiendeleza Kiswahili nchini Misri.
Pia Mhe. Balozi nae alikabidhiwa vitabu vilivyotungwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Al Azhar, kilichoanza kufundisha Kiswahili tokea Mwaka 1967. Aidha, Redio Cairo, idhaa ya Kiswahili ilianza matangazo yake mwaka 1954. Jumla ya wanafunzi 500 wanasoma Kiswahili nchini Misri ambapo 400 kati yao wapo katika Chuo cha Ain Shams.