Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri aliadhimisha kwa mara ya kwanza Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani katika ukumbi wa Umoja wa Wanafunzi wa Kimisri siku ya Ijumaa tarehe 29 Julai, 2022.   Wahadhiri, wanafunzi na wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini Misri walipata fursa ya kuwasilisha mada mbali mbali ikiwa ni pamoja na historia fupi ya kiswahili, ufundishaji wa lugha ya kiswahili nchini Misri, matumizi ya lugha ya Kiswahili, faida na changamoto za ufundishaji wake. 

Aidha,  wahadhiri hao walielezea uzuri wa lugha ya Kiswahili kuwa ni chepesi kufundisha na kujifunza, kitamu kukizungumza mfano wa mtoto asivyotaka kuliacha titi la mama yake likiwa kinywani. 

Pia,  wanafunzi wanaojifunza Kiswahili chini Misri wameifananisha lugha ya Kiswahili kama ni jua la Bara la Afrika linalotoa matumaini ya kuleta amani, umoja na maendeleo, sio tu barani Afrika bali pia duniani kote. Hii ni kwa sababu Kiswahili kinatumika kama lugha ya mawasiliano kimataifa, kinatumiwa na vyombo vya habari mbali mbali duniani kote na sasa kinafundishwa katika vyuo vikuu duniani kote.

Katika Kongamano hilo pia, Mhe. Balozi alitumia nafasi kwa kuitambulisha rasmi Tanzania – The Royal Tour kwa kuionesha kwa hadhira iliyopo huku akiwataka wasiache kuitembelea Tanzania kwa ajili ya kujionea uzuri wa mandhari na mbuga asilia zilizopo nchini.

Aidha, katika tukio hilo hilo Mhe. Balozi alipokea zawadi za Vikombe kutoka kwa timu mbili za Taifa za Tanzania za mchezo wa Kabadi (wavulana na wasichana) zilizoshiriki katika mashindano yaliyofanyika nchini Misri kuanzia tarehe  22 Julai hadi 28, 2022. 

Timu hizo zimefanikiwa kuchukua nafasi ya mshindi wa pili katika mashindao ya kimataifa yaliyoandaliwa na Chama cha mchezo wa Kabadi nchini Misri. Timu hizo pia zimepata nafasi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia litakalofanyika nchini India mwishoni mwa mwaka huu. 

Mwisho kabisa Mhe. Balozi alitoa zawadi za vyeti kwa wahadhiri wakuu, na wasimamizi  wa Kongamano hilo na kuahidi kuwa huu sio mwisho wa kufanyika kongamano bali lataendelea kila mwaka sambamba na kuwashukuru wote waliohudhuria.