Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeanza ziara yake nchini Misri tarehe 10 Agosti, 2024, kwa kutembelea Mji Mpya wa Kiutawala ambako Serikali ya Misri imehamia kuona majengo ya kisasa ya Wizara mbali mbali, Benki, Jengo refu zaidi Barani Afrika lenye ghorofa 75 na miundo mbinu ya kisasa ya makazi, barabara na njia za treni.
Aidha, waliangalia mji wa michezo, nyumba za ibada na uwekezaji unaofanywa na Jeshi la Misri katika hoteli za kisasa.
Ziara hiyo imeendelea tarehe 11 kwa kutembelea Kampuni ya Arab Organization for Industrialization iliyoanzishwa mwaka 1975 kwa ushirikiano wa Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar, ambazo ziliweka mtaji kukidhi mahitaji ya Majeshi ya nchi hizo pamoja kwa zana za kijeshi, silaha, teknolojia pamoja na uzalishaji wa mahitaji mbali mbali ya kijamii, kukidhi soko la ndani na ziada kuuza nje ya nchi.
Taasisi hiyo ni mkusanyiko wa Makampuni zaidi ya 15 ambazo zimetoa ajira kwa watu zaidi ya 15,000.
Ziara imeendelea kwa kutembelea kampuni ya National Company for Protected Agriculture inayozalisha Mazao ya matunda na mboga mboga kukidhi soko la ndani na ziada huuzwa nchi 17 za Ulaya.
Kiwanda cha Qadr Factory hutengeneza magari ya kijeshi, magari ya zimamoto, magari ya Benki na ofisi zinazotembea, magari ya wagonjwa na kusafirishia fedha yenye vifaa vya kisasa na teknolojia ya hali ya juu.
Kampuni ya Kilimo huzalisha embe, machungwa, chenza, tende, pilipili mboga na kadhalika kwa kutumia kilimo cha umwagikiaji maji na green houses.
Ziara hiyo itaendelea tarehe 12 na 13 kwa kutembelea viwanda huko Helwan kuangalia uzalishaji wa magari ya aina mbali mbali, vifaa vya kuzimia moto, vipoza hewa na kadhalika pamoja na viwanda vya Silaha.
Kamati yenye wajumbe 31 itakamilisha ziara yake nchini Misri tarehe 13 Agosti, 2024 na kurejea Tanzania tarehe 14 Agosti, 2024.
Lengo la ziara hiyo ni kujifunza kwa vitendo utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi na viwanda kupitia Sekta ya Ulinzi kwa kushirikiana na Sekta binafsi pamoja na kufahamu mchango wa Sekta ya ulinzi katika kukuza uchumi wa nchi na huduma mbali mbali za kijamii.
Kwa kiasi kikubwa Kamati imejifunza kuwa Uchumi wa Misri umeshikiliwa na Vikosi vya Ulinzi na kutoa ushindani mkubwa katika uzalishaji, hali ambayo inawapa nafuu ya maisha wananchi kwa kupunguza bei ya bidhaa mbali mbali sokoni kutokana na kuzalisha kwa wingi bidhaa za viwandani na Kilimo.