Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania alifanya ziara ya kikazi jijini Banu Suef, nje kidogo ya mji wa Cairo siku ya Ijumaa tarehe 15/04/2022 wakati wa jioni kukagua viwanda vya utengenezaji wa viungo (spices) vya majani ya vitunguu ambapo huuzwa katika hali ya unga kwa kutumika katika aina mbali mbali ya vyakula.
Soko kubwa la bidhaa hizo ni nje ya Misri kama ujerumani, Ufaransa na Marekani. Pia, alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza chakula cha wanyama mbali mbali kwa kutumia mahindi ya njano wanayoyatoa Ukraine, Moldova n.k. Kampuni ya Smart Group hivi karibuni imetiliana saini na Taasisi ya SUGECO ya Morogoro kwa uzalishaji na ununuaji wa Mahindi ya njano kutoka Tanzania, makubaliano ambayo yalitiwa saini katika Ubalozi wa Tanzania uliopo Cairo, Misri ili kuiwezesha Tanzania kuzalisha kwa wingi mahindi ya njano na kuuza moja kwa moja nchini Misri.
Hii ni fursa mpya kwa Tanzania kupata soko la uhakika la mahindi na kuibua fursa za ajira na ujenzi wa viwanda hasa utengenezaji wa vyakula vya mifugo nchini Tanzania.