Mhe Liberata Mulamula baada ya mkutano na Mhe. Sameh Shoukri, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Misri, alifika Ubalozini na kuzungumza na wafanyakazi ambapo aliutaka uongozi wa Ubalozi kufanyakazi kwa mashirikiano na kuwa kitukimoja, kuzingatia sheria za manunuzi wakati wa matumizi ya fedha za Serikali na kuacha matumizi ya Serikali kwa mambo ambayo sio muhimu na ya msingi. 

Sambamba na hayo, Uongozi wa ubalozi umekumbushwa kuzingatia umuhimu wa Ubalozi wa Misri kama ni nchi ya kimkakati sio tu kuendeleza mahusiano ya kihistoria, bali pia kwa kuimarisha mashirikiano kuleta maendeleo ya Tanzania kupitia sekta ya elimu, afya, kilimo, nishati, maji, ulinzi na usalama, mazingira na teknolojia na tafiti za kisayansi. 

Pia Balozi Liberata Mulamula alitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa ubalozi kuendelea kuzitunza vyema Mali za Serikali na kujipanga kuweza kukiendeleza kiwanja kilichotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kupewa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika eneo la mji mpya wa kiutawala, eneo la ‘New Cairo’, eneo ambalo Serikali ya Misri imelitenga kwa kuhamishia Serikali yote ya Misri, Balozi zote na Taasisi za  Kimataifa za kibalozi na Mashirika ya Umoja wa Mataifa.