Mhe. Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, alifanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Saratani ya Shefaa Al Orman Oncology Hospital iliyopo katika mji wa Luxor.
Ziara hiyo ililenga kufanya tathmini ya awali (due diligence) ili kujionea uwezo wa hospitali katika kutoa huduma za saratani na kuangalia uwezekano wa kuanzisha ushirikiano kati ya hospitali hiyo na mamlaka za afya za Tanzania, ikiwemo Wizara ya Afya pamoja na Hospitali za saratani nchini.
Katika ziara hiyo, ujumbe ulipata maelezo ya kina kuhusu uwezo wa hospitali katika utoaji wa huduma jumuishi za saratani kwa watu wazima na watoto. Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa awali wa saratani, matibabu ya kemotherapi, radiotherapi ya kisasa kwa kutumia linear accelerators, upasuaji wa saratani, uchunguzi wa radiolojia na nuclear medicine, pamoja na huduma za uangalizi maalum kwa wagonjwa mahututi (ICU).
Hospitali pia ina kitengo cha kisasa cha upandikizaji wa uboho na seli shina (bone marrow na stem cell transplant) pamoja na maabara za uchunguzi wa kijenetiki kwa mfumo wa precision oncology.
Aidha, wanatibu ugonjwa wa Kansa zote, ugonjwa ukiwa katika hatua yoyote ile, na mgonjwa akitibiwa uponaji ni asilimia 97 bila ya ugonjwa kujirudia.
