Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri uliipokea Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 (U17) iliyowasili nchini Misri kwa ajili ya kuweka kambi maalum ya maandalizi kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (afcon u17). 

Ziara hii ni kufuatia mwaliko walioupata kutoka timu ya U17 ya hapa Misri. Katika kuonesha mshikamano na kuunga mkono juhudi za vijana hao, Mheshimiwa Balozi, Mej. Jen. Richard M. Makanzo akiongozana na maafisa wa Ubalozi, aliitembelea kambi ya timu hiyo pamoja na kuhudhuria mechi za kirafiki zilizochezwa kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania U17 na Timu ya Taifa ya Misri U17. Mechi ya kwanza ilichezwa tarehe 14 Machi 2026, ambapo matokeo yalikuwa sare ya bila kufungana (0–0), na mechi ya pili ilichezwa tarehe 16 Machi 2026 ambapo Tanzania ilifungwa bao 1–0 na wenyeji, Misri.

Kufanyika kwa ziara hii ya timu yetu hapa nchini Misri ni sehemu ya juhudi za kuimarisha Diplomasia ya Michezo kupitia ushirikiano huu ambapo ushirikiano wa Kimataifa unaendelezwa sambamba na kukuza vipaji vya vijana.

 Aidha, Mheshimiwa Balozi alipata fursa kwa nyakati tofauti kuzungumza na viongozi pamoja na wachezaji wa timu hiyo, akiwapa hamasa, kuwajengea moyo na kusisitiza umuhimu wa kulipigania, kulitetea na kuliheshimisha Taifa letu. 

Kabla ya kurejea nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi alionesha moyo wa ukarimu kwa vijana hao kwa kuwapatia motisha kwa kuwaandalia ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria na kitalii ya Pyramids. Ziara hiyo imekuwa zawadi maalum na kumbukumbu ya thamani kwa vijana hao shupavu.

 Mwisho, Mheshimiwa Balozi aliwatakia safari njema na mafanikio mema, akiwatia moyo kuwa wao ni watetezi wa Taifa na ni mustakabali mwema wa nchi yetu.