Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Mhe. Balozi Meja Jenerali Richard M. Makanzo, pamoja na maafisa wa ubalozi huo katika ofisi za ubalozi.

Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Mhe. Makamba kushiriki Kikao cha 21 cha Mawaziri wa Nishati wa kikanda kinachohusu biashara ya umeme kupitia jukwaa la Eastern Africa Power Pool (EAPP).

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Makanzo alimpa Mhe. Makamba maelezo mafupi kuhusu historia na shughuli za Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, pamoja na nafasi yake katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi za ukanda huo.

Aidha, Mhe. Balozi alimtakia Mhe. Makamba mafanikio mema katika uwakilishi wake kwenye kikao hicho muhimu, akieleza matarajio kuwa kitatoa mchango chanya katika kuimarisha ushirikiano wa nishati na maendeleo ya biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki.