Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, tarehe 26 Aprili 2026, uliadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika hafla maalum iliyofanyika katika Hoteli ya Cairo Marriott jijini Cairo, Misri. 

Sherehe hizo ziliandaliwa na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard M. Makanzo, kwa ushirikiano na wawekezaji wakubwa nchini Tanzania ambao ni kampuni za Elsewedy Electric na Arab Contractors. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Mhe. Mohamed Abu Bakar Saleh Fattah, huku mgeni mwalikwa akiwa Naibu Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Salome W. Makamba. 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na mabalozi wa mataifa mbalimbali (ikijumuisha mabalozi wanaowakilisha nchi zao kanda ya EAC na SADC, vilevile mabalozi wa nchi tunazoziwakilisha; Lebanon na Libya), viongozi waandamizi wa Serikali ya Misri, wafanyabiashara, wawekezaji, wanadiplomasia, pamoja na Watanzania wanaoishi na kusoma nchini Misri.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Fattah alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Misri, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, nishati na maendeleo ya miundombinu. 

Kwa upande wake, Balozi Makanzo alieleza mafanikio yaliyofikiwa ndani ya miaka 62 ya Muungano na kupongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuvutia uwekezaji wa kimataifa nchini Tanzania.

Alibainisha kuwa diplomasia ya uchumi ni nyenzo muhimu katika kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa, hususan kwa kuzingatia nafasi ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kama lango la masoko ya Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Aidha, alisisitiza kuwa kupitia diplomasia hiyo, Tanzania imeendelea kunufaika kwa kupanua fursa za kiuchumi, kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuvutia wawekezaji kutoka Misri na kwingineko, hatua inayochangia ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya taifa.