Serikali ya Tanzania imeshiriki katika Mkutano wa 21 wa Mawaziri wa Nishati wa Afrika Mashariki uliofanyika Cairo, Misri, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika biashara ya umeme kupitia Eastern Africa Power Pool (EAPP).

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, akishirikiana na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Meja Jenerali Richard Makanzo. Viongozi wengine waliojumuika ni Kamishina Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Mhandisi Styden Rwebangila, pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Anthony Mbushi, wakisaidiwa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na EWURA.

Mkutano ulijikita katika ajenda kuu tatu: kuharakisha uanzishwaji wa soko la pamoja la umeme la kikanda, kuimarisha miundombinu ya kuunganisha gridi za nchi wanachama, na kuweka mifumo ya kisheria na kiutendaji itakayorahisisha biashara ya umeme baina ya nchi. Pia ulijadili nafasi ya Misri kuwa mwenyeji wa kituo cha uendeshaji wa soko hilo, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uwazi wa biashara ya umeme katika ukanda.

Kwa Tanzania, ushiriki huu una faida za kimkakati ikiwemo kupanua soko la umeme unaozalishwa nchini, kuongeza mapato ya sekta ya nishati, na kuimarisha usalama wa upatikanaji wa umeme kupitia ubadilishanaji wa nishati na nchi jirani. Aidha, unaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa mdau muhimu katika uchumi wa nishati wa kikanda na kuvutia uwekezaji zaidi katika miundombinu ya umeme.