Mhe. Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, alifanya ziara ya kikazi katika mji wa Luxor, ambapo alipata fursa ya kukutana na Gavana wa mkoa huo, Abdel Motaleb Mamdouh Emara. Lengo la ziara lilikuwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, kijamii na kiutawala kati ya Tanzania (hususan Zanzibar) na mkoa wa Luxor nchini Misri.


Katika mazungumzo kati ya Mhe. Balozi na Gavana wa Luxor, pande zote mbili zilitambua fursa zilizopo za ushirikiano kati ya Luxor na Zanzibar. Ilisisitizwa kuwa miji yote miwili ina sifa zinazofanana, ikiwemo kuwa na historia ya kale na kuwa vivutio vikubwa vya utalii. Aidha, Zanzibar imetajwa kuwa moja ya maeneo yanayopendwa na watalii wa Misri, jambo linalotoa msingi mzuri wa ushirikiano wa sekta ya utalii.


Pande hizo mbili zilikubaliana kuanzisha mipango ya ushirikiano katika maeneo yafuatayo:
• Utalii: Kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa vivutio vya kihistoria na kukuza utalii wa kimataifa.
• Kilimo: Ushirikiano katika uzalishaji wa mazao ya biashara kama miwa na nyanya pamoja na teknolojia za uchakataji wa mazao.
• Huduma za Afya: Kubadilishana uzoefu na utaalamu katika huduma za hospitali, hususan magonjwa ya saratani nna afya ya uzazi.