Mnamo tarehe 17 Februari 2026, Mheshimiwa Mej. Jen. Richard M. Makanzo Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, akiambatana na Maafisa wa Ubalozi, aliwapokea rasmi wanafunzi saba wapya waliowasili kutoka Tanzania kwa ajili ya kuanza masomo yao ya juu katika Vyuo Vikuu vya German University in Cairo (GUC) na German International University (GIU).
Mapokezi hayo yalifanyika katika mazingira ya kirafiki na ya kuhamasisha, ambapo Mheshimiwa Balozi aliwapongeza wanafunzi hao kwa kuchaguliwa kujiunga na vyuo hivyo vyenye hadhi ya kimataifa. Aidha, aliwahimiza kuzingatia masomo yao, kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania, na kutumia fursa hiyo kujenga taaluma na mahusiano yatakayowanufaisha wao binafsi pamoja na Taifa kwa ujumla.
Vyuo hivyo ni vya sekta binafsi na ni vyuo adhimu, hususan katika masomo ya kisayansi. Wanafunzi walioteuliwa wamepata ufadhili kamili wa masomo (full scholarship), jambo linalodhihirisha dhamira ya dhati ya kuwainua kitaaluma katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Mafanikio ya kupatikana kwa nafasi hizo yamekuja kufuatia ufuatiliaji wa karibu na maombi maalum yaliyofanywa na Ubalozi katika kuhakikisha Watanzania wanapata fursa zaidi za kielimu katika vyuo vya kisayansi. Hii ni juhudi mahsusi za Mheshimiwa Balozi katika kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa fursa hizo muhimu kwa vijana wa Kitanzania.
Kwa upande wa Ubalozi, umeahidi kuendelea kushirikiana na wanafunzi hao katika kipindi chote cha masomo yao ili kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi.


