Mhe. Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard M. Makanzo, ameshuhudia maandalizi ya Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, inayojiandaa na mashindano ya WAFCON yanayotarajiwa kufanyika nchini Morocco tarehe 17 Machi hadi 03 Aprili, 2026. Timu hiyo iliwasili Misri tarehe 16 Februari 2026 kwa ajili ya kuweka kambi maalum ya maandalizi, ambapo tayari imecheza michezo miwili ya kirafiki. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa tarehe 20 Februari 2026 dhidi ya Timu ya Mkoa wa Ismailia, Twiga Stars iliibuka na ushindi mnono wa mabao 16–0. Mchezo wa pili uliopigwa tarehe 24 Februari 2026 dhidi ya ZED FC ulimalizika kwa ushindi wa bao 1–0 kwa upande wa Twiga Stars. 

Baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya ZED, Mhe. Balozi alipata fursa ya kuzungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi na kusisitiza umuhimu wa kulipigania Taifa kwa moyo wa kujitolea. Alieleza kufurahishwa na kiwango kizuri kinachooneshwa na timu pamoja na nidhamu ya kufuata maelekezo ya makocha. Aidha, aliwatakia mafanikio mema katika maandalizi yao na kuwahakikishia kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Misri uko tayari kutoa ushirikiano wowote watakaohitaji. 

Twiga Stars inatarajiwa kuondoka nchini Misri tarehe 25 Februari 2026 kuelekea Dubai ili ishiriki mashndano madogo yanayojulikana kwa jina la Pink Ladies yaliyo chini ya uangalizi wa FIFA, ambapo itacheza dhidi ya timu za Urusi, Hong Kong na Ghana ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea WAFCON.