Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri katika juhudi za kutafuta Wawekezaji, ametembelea Ofisi za Kampuni ya Mijo Auto PVT Co. Ltd yenye Makao Makuu yake nchini India kuona utendaji na Maendeleo ya Kampuni hiyo katika tawi lake nchini Misri.

Kampuni hii imeanzishwa mwaka 2001 kutoa huduma za utengenezaji wa vipuri vya magari kuwezesha kutumia nishati ya gesi badala ya Petroli.

Kampuni inafanya kazi na Kampuni ya  Taqa Arabia na GB Corp zote za Misri. Kampuni ya Mijo inakusudia kufanya kazi zake nchini Tanzania kwa uwekezaji wa kiwanda cha kutengeneza vipuri hivyo pamoja na kuingiza teknolojia hiyo ya kutengeneza vipuri hivyo kwa kushirikiana na Dar es Salaam Institute of Technology, SUMA JKT na TPDC.

Wakati huo huo Mhe. Balozi alitembelea Chuo cha ufundi wa magari kinachomilikiwa na Kampuni ya GB Corp. ambacho hutoa mafunzo ya ufundi wa magari, fani za mashine, umeme, rangi, na ukatabati wa magari ya aina mbali mbali.

Kampuni ya GB Corp. Inawasilisha makampuni zaidi ya 35 Duniani kote yanayotengeneza magari na vilainishi vya magari. Pia, Kampuni inatengeneza na kuunganisha magari kupitia viwanda vyake vilivyopo maeneo tofauti nchini Misri.

Aidha, Kampuni ina taasisi yake ya kiraia inayotekeleza miradi mbali mbali ya kijamii ili kurejesha faida katika jamii. Kampuni hii imeajiri zaidi ya wafanyakazi 20,000 na kuendesha Shule mbali mbali za ufundi.

Kampuni inakusudia kuingia soko la Tanzania kwa uwekezaji na kusambaza elimu ya ufundi kwa kushirikiana na Taasisi za elimu za Ufundi nchini Tanzania kwa kubadilishana uzoefu na wanafunzi wa Tanzania kupatiwa nafasi katika vyuo vya Kampuni hiyo.