Tarehe 06 Machi 2026, Mhe. Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, akiambatana na baadhi ya Maafisa kutoka ubalozini, alihudhuria na kushiriki katika hafla ya futari iliyoandaliwa kwa ajili ya Watanzania wanaoishi katika mkoa wa Alexandria.
Hafla hiyo iliwakutanisha pamoja Watanzania mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa, wanafunzi wanaosomea taaluma tofauti, wanajeshi pamoja na wanadiaspora wanaoishi na kusoma katika mkoa huo.
Katika hafla hiyo, Mhe. Balozi alipata fursa ya kusikiliza hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Alexandria ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Diaspora nchini Misri Bw. Genarld Kalinga, ambapo aliwasilisha maoni, matakwa pamoja na changamoto zinazowakabili wanafunzi na Watanzania wanaoishi katika eneo hilo.
Kufuatia hotuba hiyo, Mheshimiwa Balozi alitoa mrejesho na kuahidi kuwa ofisi yake itafanyia kazi maombi na mapendekezo yaliyowasilishwa.
Aidha, Mheshimiwa Balozi alitoa nasaha na ushauri kwa wanafunzi na Watanzania waliokuwepo, huku akisikiliza kwa makini changamoto mbalimbali walizozieleza. Alisisitiza kuwa ubalozi utaendelea kushirikiana nao kwa karibu na kuwasilisha changamoto hizo katika mamlaka husika, iwe ni za nchini Misri au Tanzania, ili kutafuta ufumbuzi wake.
Mhe Balozi aliwahakikishia kuwa wako salama na Misri kwa ujumla iko salama kufuatia Vita inayoendelea katika ukanda huu, na kuwataka wote wajiandikishe kwenye platform ya diaspora na kwamba Ubalozi ndio utatoa taarifa sahihi na kwamba waendelee kufuata maelekezo ya Serikali ya hapa endapo yatatolewa.
Vilevile, Mhe. Balozi alishiriki futari ya pamoja iliyoandaliwa na Ubalozi kwa kushirikiana na wanafunzi na Watanzania waliopo Alexandria, hatua iliyolenga kuimarisha mshikamano na mawasiliano kati ya Ubalozi na raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi.
Katika hitimisho lake, Mhe. Balozi alisisitiza umuhimu wa Watanzania waliopo nje ya nchi kutumia vyema nafasi na fursa walizonazo, akieleza kuwa wao ni tegemeo muhimu la taifa la Tanzania la sasa na la baadaye kupitia taaluma, maarifa na uzoefu wanaoupata.
Hafla hiyo ilimalizika katika hali ya ushirikiano, umoja na mshikamano, huku Watanzania waliokuwepo wakionesha shukrani kwa ubalozi kwa kuendelea kuwajali na kushirikiana nao.
Mwisho wa hafla hiyo ulihitimishwa kwa dua ya pamoja ya kuliombea Taifa la Tanzania, Viongozi wake pamoja na kuendelea kudumisha umoja, amani na mafanikio ya nchi.





