Tarehe 29.10.2026 Mhe. Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard M. Makanzo, akiambatana na Mwambata Biashara na Mwambata Fedha, alishiriki katika maadhimisho ya kuwakumbuka mashujaa waliofia vitani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia katika eneo la Mashariki ya Kati (mwaka 1943 hadi 1944), yaliyofanyika katika makaburi ya mashujaa wa vita ya Fayid War Cemetery (Suez Canal). 

Maadhimisho hayo yaliandaliwa kwa pamoja na Ubalozi wa Ubelgiji na Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yakihudhuriwa na Mhe. Éliézer Ntambwe Mposhi, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Wastaafu wa Kijeshi katika Wizara ya Ulinzi ya DRC, kama mgeni rasmi, pamoja na Mabalozi mbalimbali toka Afrika, Ulaya, Asia, Amerika  na Viongozi wa Serikali ya Misri.

Katika kuendeleza juhudi za kuhifadhi historia, Ubalozi wa Tanzania umebaini baadhi ya majina ya wapiganaji kutoka Tanzania waliopigana vita hivyo wakiwa chini ya Afrika Mashariki waliofariki wakati wa vita hivyo na kuzikwa nchini Misri. 

Ubalozi unalenga kufanya utafiti zaidi ili kubaini majina ya wapiganaji wote kutoka Afrika Mashariki waliozikwa katika makaburi ya kihistoria yaliyopo Alexandria, Heliopolis jijini Cairo na Fayid, eneo la Suez, kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu zao na kuanzisha utaratibu wa kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa hao wa Afrika Mashariki.