Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Mej. Jenerali Richard M. Makanzo, amepokea katika Jiji la New Alamein, Misri, Ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Nane wa AU Mid-Year Coordination Summit pamoja na El Alamein Africa Forum. Mhe. Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mikutano hiyo inayowakutanisha viongozi waandamizi wa Afrika kujadili masuala ya maendeleo, ushirikiano wa kikanda na ajenda za bara.
Mikutano hiyo imeanza 02 Oktoba 2026 katika Jiji la New Alamein chini ya kaulimbiu “Africa on the Land of El Alamein”, na inaendelea hadi 04 Oktoba 2026, wakati Mkutano wa AU Mid-Year Coordination Summit ukitarajiwa kufanyika tarehe 04 Oktoba 2026.
Ujumbe wa Tanzania unashiriki pamoja na viongozi wengine wa Afrika katika kujadili na kuendeleza ajenda za ushirikiano wa Afrika, maendeleo endelevu, biashara na uwekezaji, utekelezaji wa Agenda 2063, amani na usalama pamoja na ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa wa Bara la Afrika.




