Mhe. Balozi Meja Jenerali Richard M. Makanzo, Balozi wa Tanzania nchini Misri, amempokea Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb.), ambaye anaiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Aswan kuhusu Amani na Maendeleo Endelevu, unaofanyika tarehe 21–22 Novemba 2026, mjini Aswan, Misri. Mhe. Balozi ameambatana na Naibu Waziri katika kushiriki mkutano huo.
Mkutano huo, unaobeba kaulimbiu “Redefining Global Commons: Africa’s Agency in an Age of Disruption”, unajadili nafasi ya Afrika katika kukabiliana na changamoto za kimataifa, hususan amani na usalama, usalama wa Bahari ya Shamu na Pembe ya Afrika, usalama wa chakula, biashara na minyororo ya ugavi, ugaidi, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na matumizi ya teknolojia mpya na akili unde (AI) katika kukuza maendeleo.
Mkutano unatarajiwa kuhitimishwa kwa kupitisha “Aswan Conclusions”, yatakayoweka mapendekezo na vipaumbele vya pamoja kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, mageuzi ya mifumo ya utawala na ufadhili wa maendeleo, ujenzi wa amani na ustahimilivu wa Afrika. Maazimio hayo yataongoza utekelezaji wa hatua mahsusi kupitia ushirikiano wa Serikali, Umoja wa Afrika na wadau wa maendeleo.
Ushiriki wa Tanzania unaimarisha dhamira ya nchi katika diplomasia ya kimataifa, kulinda maslahi ya Afrika na kukuza amani na maendeleo endelevu.






