Tarehe 26.06.2026, Mhe. Maj Gen Richard Makanzo, Balozi wa Tanzania nchini Misri, alishiriki katika hafla ya kufunga mwaka ya Hospitali ya Nile of Hope Pediatric Surgeries & Congenital Anomalies Hospital iliyofanyika Alexandria, Misri.
Katika hafla hiyo, uongozi wa hospitali uliwasilisha mafanikio makubwa ya taasisi hiyo katika kutoa huduma za kibingwa za upasuaji na matibabu kwa watoto wenye matatizo ya kuzaliwa, ambapo maelfu ya watoto wamefikiwa na huduma hizo tangu kuanzishwa kwa hospitali.
Mhe. Balozi Makanzo alipongeza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Nile of Hope Hospital, ikiwemo kambi za matibabu ya watoto zilizowahi kufanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kunufaisha watoto wa Kitanzania pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya.
Aidha, ilielezwa kuwa wazo la jina la “Nile of Hope” lilipata msukumo kutoka Tanzania, ambako chanzo kikuu cha Mto Nile ni Ziwa Victoria, likiwa ishara ya matumaini, uhai na mshikamano wa watu wa Bonde la Nile na Afrika kwa ujumla.
#TanzaniaMisri #NileOfHope #DiplomasiaYaAfya #AfyaKwaWatoto



