Mhe. Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi siku ya tarehe 12/09/2022 akiambatana na Afisa wa Ubalozi Mhe. Suleiman R. Haroun walifanya ziara ya kikazi mkoani Buheira kutembelea kiwanda cha Al Saratex kinachojihusisha na utengenezaji wa nyuzi na nguo. 

Kiwanda hicho kinamilikiwa na ndugu wawili, Bw.  Eng. Mohamed Mousaad na Bi. Sara Mousaad. Katika maongezi yake mhe. aliwaeleza umuhimu na nafasi za kipekee zilizopo nchini Tanzania ikizingatiwa kuwa ni lango kuu na eneo muwafaka la kuwezesha biashara itambulike kirahisi katika nchi zinazoizunguka Tanzania. 

Aidha,  wawekezaji hao walimjulisha Balozi kuwa bidhaa zao zinauzwa pia nchini Tanzania lakini zinaingia kupitia nchi zingine za jirani na kuwa wana mkakati wa kuanza kwanza kuuza moja kwa moja Tanzania ikiwa ni hatua ya kuanzia kabla ya kufikiria kuanzisha kiwanda. Pia walimjulisha Balozi Nchimbi bidhaa zao ni malighafi inayotumika kwa viwanda vidogo na vikubwa hivyo vinasaidia kutengeneza kuongezwa thamani ndani ya nchi hivyo kukuza kipato na ajira.

Halikadhalika,  Mhe. Balozi alijionea jinsi nyuzi hizo zinavyotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, "Nimeridhishwa sana na ubora wa kiwanda chenu na uzalishaji unaofanyika, hivyo, nawaomba  kuitumia fursa ya kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri kwa wewekezaji" Alisema. 

Mwisho kabisa, Mhe. Balozi alitoa shukurani zake kwa wenyeji wake na kuwapa zawadi za ngao zenye kuonesha maeneo ya utalii nchini Tanzania, ikiwa ni mojawapo ya kutumia fursa za kutangaza utalii nchini.