Mhe. Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Leo tarehe 16 Agosti, 2024 amefika viwanja vya Jewel Sports City, New Cairo kuonana na Viongozi na Wachezaji wa Timu ya JKU Sports Club ya Zanzibar iliyowasili Cairo, Alfajiri ya Siku ya Ijumaa tarehe 16 Agosti, 2024 kwa Kuweka kambi kabla ya mechi yao dhidi timu ya Pyramids ya Misri kugombania nafasi katika mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika.

Mheshimiwa Balozi aliwakaribisha Viongozi na Wachezaji ya timu ya JKU nchini Misri na aliwataka wachezaji kujituma, kutumia fursa hiyo kuonyesha uwezo wao katika mchezo wa mpira kwa kuwa mpira sasa ni ajira na vilabu vikubwa duniani hutafuta wachezaji kupitia mashindano kama hayo.

Aidha, aliwatakia mafanikio timu ya JKU katika michezo yao ambapo mechi ya kwanza itachezwa siku ya Jumapili tarehe 18 Agosti, 2024 saa 2 usiku katika uwanja wa 30 June Stadium uliopo New Cairo.

Vile vile, aliwataka wachezaji kutumia vyema nafasi katika dakika za mwanzo katika mashindano hayo ili kuwapa mshangao timu ya Pyramids hali ambayo itawasaidia kujihakikishia ushindi katika mashindano hayo.

Mheshimiwa Balozi aliwahakikishia Viongozi na wachezaji wa Timu ya JKU Sports Club kwamba uwezo wa kushinda katika michuano hiyo ni mkubwa iwapo vijana hao watatulia, kujituma na kuonyesha uwezo wao katika kusakata soka, na kwamba Ubalozi uko pamoja nao na Watanzania waliopo Misri watafika kwa wingi kuwapa hamasa ya ushindi katika mashindano hayo.